Somo kwanza, Mdo 2:1-11
Somo Pili, Rum 8:8-17
Injili, Yn 20:19-23
Somo kwanza, Mdo 2:1-11
Somo Pili, Rum 8:8-17
Injili, Yn 20:19-23
Utangulizi
Pentekoste ni siku hamsini baada ya Pasaka. Ni kuzaliwa kwa Kanisa. Roho Mtakatifu anamiminwa juu kanisa. Ni mwendelezo wa kazi ya Kristo katika maisha yetu. Pentekoste ni udhihirisho wa hadhara wa Kristo. Ni siku ya utimilifu wa ufunuo wa Utatu Mtakatifu.
Homilia
Pentekoste ni utimilifu wa mafumbo ya Pasaka katika maisha ya Kanisa. Kanisa linajaliwa zawadi ya Roho Mtakatifu, amabaye ni Mfariji, Mshauri wa kweli, Chanzo cha nguvu ya utume wa kutangaza Injili. Hivyo sit u sherehe, bali tunapewa nguvu ya kuishi na kutangaza Injili kwa ujasiri, upendo na hekima.
Somo la I
Kitabu cha Matendo ya Mitume katika somo la kwanza kinatuelezea jinsi ndimi za moto zilivyowashukia mitume. Nao walikuwa wakisema kea lugha nyingi. Lugha hii ya Kipentekoste sio lugha ya kupingana, sio lugha ya kutokuelewana, sio lugha ya kuwachanganya watu, sio lugha ya kuwapotosha watu, sio lugha ya kuwaficha watu. Ni zawadi ya Roho Mtakatifu ya Lugha ya Kuelewana, kuwasiliana, kuwa kitu kimoja. Hivyo roho anayetuleta pamoja kama Kanisa, kama Wakristo, kama wabatizwa, kama wanafamilia ya Mungu, kama wanadamu, kama wanajamii, kama wana taifa moja. Kinachotufanya tunashindwa kuwa kitu kimoja, kusema lugha moja kama kanisa, jamii, na taifa ni nini wakati tumempokea Roho Mtakatifu?. Kitabu cha Mwanzo sura ya 11, inatuambia watu wote walikuwa taifa moja na lugha moja. Lakini kilichowasambaratisha ni nini? Kubishana na Mungu, kutaka kutengeneza mnara ufike kwa Mungu, kujivuna, kutokutambua nafasi ya Mungu katika maisha yao, kutumia vibaya nguvu zao na vipaji vyao, kutaka umaarufu, kutaka madaraka.
Somo la II
Mtume Paulo anatuambia kuwa na karama tofauti si shida, vipaji tofauti ni zawadi ya huyo Roho Mtakatifu tuliyempokea. Matumizi mabaya ya karama, uwezo, mamlaka, nyadhifa, vipaji, elimu, madaraka ndio shida. Matumizi hayo mabaya ya karama za Roho ndio matokeo ya Vita, dhuluma, unyanyasaji, ufisadi, rushwa, uchu wa madaraka, kutokutenda haki, unyanyasaji, n.k. Paulo anasema Karama mbalimbali tunazopokea kwa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya Kufaidiana. Kama vile mwili ni mmoja na viungo ni vingi basi hakuna kiungo kinachoweza kujisifu dhidi ya kingine. Maana vyote vinategemea kichwa Kimoja, yaani Kristo Yesu.
Injili
Yesu anawavuvia mitume Roho Mtakatifu. Anawapa uwezo wa kuendeleza kazi ya wokovu hasa katika kuipokea huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu katika kusamehe dhambi ndiko kunakodhihirisha mamlaka ambayo Yesu aliyowapa mitume na waandamizi wao ya kuwaondolea watu dhambi. Kitu kinachotuunganisha na Mungu ni Roho Mtakatifu. Tunapompokea Roho Mtakatifu katika ubatizo tunaunganishwa na Mungu. Kwa namna gani! lazima kuondolewa dhambi. Zawadi kubwa tunayoipata kwa Roho Mtakatifu ni Huruma ya Mungu kupitia Msamaha wa dhambi. Kanisa limepewa mamlaka hayo ya kutupa msamaha wa dhambi. Uhai wetu wa kiroho unahuishwa tena tunapopata msamaha wa dhambi zetu kupitia sakramenti ya Kitubio kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Yesu amewapa wanafunzi wake mamlaka ya kuendeleza utume wake wa kuwapatanisha watu na Mungu kwa zawadi ya Roho Mtakatifu. Hivyo Pentekoste ni kuwa kitu kimoja kama mwili wa Kristo, kama kanisa, kama taifa, kama watu wa Mungu kama wanadamu. Na zaidi kuomba Msamaha ili kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Roho Wake.