Somo la Kwanza, Isa 66:10–14
Somo la Pili, Gal 6:14–18
Somo la Injili, Lk 10:1–12, 17–20
Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenye kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apelike watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa Amani, Amani yenu itamkalia; la, hayumo, Amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wowote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yenu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.
Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahaini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.
Kristo anatualika na kutushirikisha utume wake wa hapa duniani. Aliwatuma 70 waende ule alikokusudia kwenda mwenyewe. Kwa ubatizo wetu tunashirikishwa ukuhani, unabii na ufalme wa Yesu. Yesu anatualika tuwe watenda kazi katika shamba lake.
Somo la I: Katika somo la kwanza, nabii Isaya awatia moyo Waisraeli baada ya kuteseka utumwani Babeli. Waisraeli wamekwisha rudi Yerusalemu. Wanafurahia kurudi kwao.
Tunapotubu dhambi tunarudi nyumbani, tunarudi katika muunganiko na Mungu. Tunatoka katika utumwa wa dhambi. Ndio furaha ya kweli. Pili, tunapokuwa katika shida fulani ama changamoto ya maisha na kuvushwa na Mungu ni furaha kwetu. Tatu tunaalikwa kufurahi kwa sababu Mungu ametuvusha mengi katika maisha yetu. Hakuna mtu ambaye Mungu hajamvusha katika jambo fulani; ugonjwa, hatari, janga fulani, changamoto ya kiuchumi, n.k. Hivyo tunaalikwa kufurahi.
Somo La II: Kitu pekee kilichotuvusha katika jambo fulani gumu katika maisha ni Msalaba wa Kristo. Paulo anatuambia hakuna kitu kingine anachoona fahari isipokuwa Msalaba wa Kristo. Yesu ametuvusha katika mengi. Tuna kila sababu ya kujivunia msalaba wa Kristo. Msalaba ndio Pekee unaotuonyesha njia. Ndio pekee unaotufikisha kule ambako Yesu mwenyewe amekusudia kwenda.
Injili: Msalaba wa Kristo ndio unaotutambulisha kuwa tu watenda kazi kweli katika shamba la Mungu.
- Msalaba wa Kristo ndio silaha pekee ya kumchapia mbwa mwitu katika maisha Yetu.
- Msalaba wa Kristo ndio silaha pekee katika utume wetu, wala si mfuko, mkoba, viatu, wala fedha wala mali.
- Msalaba wa Kristo ndio silaha pekee ya kushinda maradhi yote. Ndio silaha ya kuponya wagonjwa.
- Msalaba wa Kristo ndio unaotupa amani ya kweli. Ndio unaotufungulia ufalme wa mbinguni.
- Pepo watatutii na kutoka katika Msalaba wa Kristo. Hawana nguvu dhidi ya msalaba wa Kristo.
- Msalaba wa Kristo ndio utakaotuokoa na adhabu ya hukumu ya mwisho. ndio utakaotustahilia kuupata ufalme wa Mungu.
Kwa msalaba wa Kristo tumepewa uwezo wa kukanyaga nge na nyoka, na nguvu zote za adui. Ndio uliomporomosha shetani kutoka mbinguni kama umeme.
Hivyo, tuone fahari juu ya Msalaba wa Kristo. Tusione aibu kuuabudu msalaba wa Kristo. Tusione aibu kutumia msalaba katika familia zetu. Tusione shaka kusali mbele ya Msalaba wa Kristo. Tunapopatwa na majaribu tuutazame msalaba wa Kristo. Tunapopotea njia, tuutazame msalaba wa Kristo. Hivyo tuone fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo.