Somo la Kwanza: Mwa 18:20-32
Somo la Pili: Kol 2:12-14
Somo la Injili
Lk 11:1-13
Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni]. Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie maiaribuni [lakini tuokoe na vule mwovu]. Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafifi yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa. nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?
Utangulizi:
Ndugu zangu wapendwa leo Yesu anatufundisha namna ya kusali na shule ya sala. Yesu anatuhakikishia kwamba tunaposali kwa imani na kwa kunuiya Mungu anasikiliza sala zetu. Sala ya Bwana ina nguvu ya kutukutanisha na Baba na kutuweka pamoja kama watoto wake tusipoisali kwa mazoea.
Homilia:
Katika maisha yetu ya ukristo tunaweza kujikuta kukata tamaa ya kusali kwa kisingizio kwamba, ‘nimesali sana lakini sifanikiwi.’ Sio kweli sio kwamba tumesali sana hatufanikiwi, bali pengine katika kusali kwetu tumekuwa tukitamka na kuhudhuria sala kwa mazoea pasipo kusali.
Hebu jiulize, je ulishawahi kumwomba Yesu akufundishe kusali, kama huyu mwanafunzi aliyeomba Yesu awafundishe kusali? Pengine ndio, lakini ulitumia sala gani? ama namna gani kusali?
Yesu anatufundisha sala ya Bwana “sala ya Baba Yetu”. Si ngeni masikioni mwetu. Lakini, Tunaisalije? Tunatambua uzito na ukaribu wa ndani ambao sala ya Baba yetu unatuingiza kati ya sisi na Mungu Baba na sisi kwa sisi? Hili hatuwezi kulitambua na kuliona kama tunaisali kwa mazoea.
Sala ya Baba Yetu kwa ufupi tunaweza kuigawa sehemu kuu mbili. Maombi matatu ya mwanzo yanalenga uhusiano wetu na Mungu.
Kwanza kwa kutamta neno Baba “yetu” tunajiweka kwenye kundi la kuwa sisi sote ni watoto wa huyo Baba mmoja wa mbinguni. Hii imedhihirishwa pia katika somo la I pale ambapo Mungu anawahurumia watoto wake wote kwa mtoto mwenye haki mmoja. Mungu hatawaangamiza waovu kwa sababu ya mwenye haki mmoja. Hii ndio maana Mungu anaruhusu tuendelee kuwepo; tunaponea kwenye huruma ya Mungu kwa sababu ya mwenye haki mmoja. Katika Somo la II, Kristo ndiye mwenye haki mmoja anayetufanya sisi tuhesabiwe wenye haki. Na kwa Ubatizo sote tuna kuwa watoto wa Mungu na kudhubutu kumwita Mungu “Baba Yetu”.
Pili, sote tunakiri kuja kwa ufalme wake. Kwamba Mungu ndiye mtawala, ndiye mfalme wa mbingu na dunia. Tatu, kujikabidhi kwa Mungu, pindi tunaposema utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Tunaweka kila kitu mikononi Mwake.
Maombi mengine manne yaliyobaki yanalenga uhusiano wetu sisi kwa sisi. Kwanza kuomba riziki kwa pamoja, na sio kwa ubinafsi. Kuomba msamaha unaoombwa kwa kuweka ahadi ya kusamehe na sisi waliotukosea. Kuombeana kushinda majaribu na magumu kwa pamoja na kushinda vishawishi. Pamoja na kumshinda shetani kwa pamoja. Haya maombi japo kwa kifupi kabisa tukiyatazama ni kwamba tunatamka kwa mazoea bila kuishi kilichopo kwenye sala yenyewe, kwan tunaisali kwa mazoea.
Tunapoisali sala ya Baba Yetu kwa kuitafakari, kwa ibada na bila mazoea kwa hakika: Tukiomba tutapata, tukibisha tutafunguliwa, tukitafuta tutaona, tukiomba Mkate tutapewa mkate, tukiomba samaki tutapewa samaki. Kwa nini sisi tunapewa jiwe badala ya mkate au nyoka badala ya samaki? Nakupa jaribio. Sali Sala ya Baba Yetu na kuimaliza kwa kuitafakari, bila kuwaza chochote ama mwingiliano wa mawazo, ama mtawanyiko wa mawazo, Ukifanikiwa basi utajua Mungu ni mwaminifu lakini sisi wanadamu sio waaminifu na wadumivu hasa katika kuomba.
Mtakatifu Thoma wa Akwino alisema sala ya Bwana ni sala bora na kuu kuliko sala zote kwa sababu inakidhi vigezo vitano vya sala bora:
- Confident: Uhakika wa kile unachokiomba na kuamini (Ebr 4:16; Yak 1:6)
- Right: Kuomba kitu sahihi kwa Mungu (Yak 4:3)
- Well-Ordered: Yenye mpangilio wa Kimungu, unaotambua uwepo wa Mungu na baadae mahitaji ya kibinadamu (Mt 6:33)
- Fervent: Yenye msukumo wa ndani, isiotawaliwa na maneno matupu na mengi, sio ya kupayuka payuka (Mt 6:7)
- Humble: Yenye unyenyekevu. sala ya mnyenyekevu hupenya mawingu.