Somo la Kwanza: Mhu 1:2; 2:21–23
Somo la Pili: Kol 3:1–5, 9–11
Somo la Injili:
Lk 12:13–21
Mtu mmoja katika mkutano alimwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyonavyo. Akawaambia mithali akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limeza sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule , unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.
Utangulizi:
Ndugu zangu wapendwa, leo Mungu anatukumbusha kuhusu kuhangaikia mambo ya Mbinguni. Ufalme wa Mungu kwanza. Fahari za kidunia hudumu kwa kitambo kidogo sana. Mambo ya kimwili, mambo ya kidunia na fahari zake yana mwisho. Masomo yetu yanatuzamisha katika upendo kwa Mungu kwanza.
HOMILIA
Jicho halijawahi kutosheka kuona, wala sikio halijawahi kutosheka kusikia, wala tumbo halijawahi kutosheka chakula. Hivi ni viashiria kuwa kamwe hatuwezi kurizisha mambo ya mwili na ya dunia hii.
Somo la I
Utajiri na starehe za ulimwengu huu haziwezi kutuletea starehe ya kweli. Ni ubatili mtupu. Muhubiri anatuonya kuhusu starehe na maisha ya kidunia kwamba ni ya muda tu. Pengine huyu mtu alikuwa na mali nyingi alikuwa na starehe za kila aina, lakini hakupata furaha ya kweli.
Ndugu zangu wapendwa, Kitabu cha Mhubiri leo kinazungumza nasi:
- Fahari za Dunia hii zunatunyima usingizi- watu hawapati usingiz kwa sababu ya pesa na fahari
- Ndugu kwa ndugu wanagombana sababu ya ardhi, mali, pesa urithi n.k.
- Watu wanateseka kwa vita kwa sababu ya mali, madini, utajir n.k
- Watu wanadhulumiwa haki zao kwa sababu ya mali, utajiri, madaraka, fahari n.k.
- Watu wanamsahau kabisa Mungu kwa sababu ya mali, biashara, madaraka, fahari n.k
Mhubiri anasema ubatili mtupu, ubatili Mtupu. Kila kitu ni ubatili tusipotafuta kwanza ufalme wa mbinguni, tusipokuwa na hofu ya Mungu katika kumiliki vitu. Ndio maana Mwinjili Mathayo anasema “heri ninyi mlio maskini” (Mt 6:20).
Injili
Katika somo la Injili Yesu anatutahadharisha kujilinda na ‘Choyo’ ‘greed, avarice’; tafsiri yake ni uchu wa mali, uchu wa utajiri, uchu wa fahari ya kidunia.
Hata uwe na fahari kubwa kiasi gani, uwe na mali nyingi kiasi gani, hata uwe tajiri kiasi gani, haiwezi kununua uhai. Uhai ni zawadi pekee ambayo ndio utajiri tulionao kutoka kwa Mungu. Na zaidi sana hakuna mali yoyote ya kidunia itakayoweza kuokoa roho yako. Roho zetu zitaokolewa tu tukijiwekea hazina mbinguni, tukiwa maskini wa roho, tukimtumainia
Mungu, tukitumia tulivyonavyo kwa kumtukuza Mungu na kusaidiana sisi kwa sisi.
Tajiri huyu anakosa kumshukuru Mungu kwa mazao aliojaliwa kwa kuzamisha moyo wake katika fahari hiyo ya kidunia. Kristo anaungana na Mhubiri kusema ni ubatili Mtupu ubatili Mtupu; mali zake haziwezi kuokoa roho yake inayotakwa na Mungu.
Mali na fahari za kidunia si shida. Mungu ameziweka kwa ajili ya kumtukuza. Shida inatokea kwenye mali na fahari za kidunia kwa sababu zifuatazo:
- Dhuluma: Pale mali zinapopatikana kwa dhuluma na kutokugawiwa kwa haki. Tuone mfano wa mtu anayeomba Yesu akagawe urithi. Pengine ndugu yake amemdhulumu na kuona ndugu anafaidi zaidi.
- Choyo: Mioyo inapozama kwenye mali inabebwa na uchu wa mali. Tunaweka matumaini na usalama wetu katika mali, na kusahau kwamba usalama wetu upo mikononi mwa Mungu.
- Majivuno na Kiburi: Tazama tajiri wa kwenye somo la Injili, anavyojisifia na nafsi yake kuhusu mali zake. Anasahau hata Mungu aliyemjalia mali hizo
- Ubinafsi: Hata baada ya kukosa pa kuweka mavuno yake hakuwaza kugawa kwa ndugu ama wahitaji. Wala hakuwaza kutoa shukran kwa Mungu.
Yesu anatukumbusha leo kwamba mambo hayo yanatuweka mbali na ufalme wa Mbinguni. Anatukumbusha kwamba vitu tunavyojaliwa vituzamishe kwenye maisha ya umilele. Tusimezwe na mali na starehe za hapa duniani.
Tunaalikwa kutambua jambo moja tu.
Katika Somo la II: Mtume Paulo anatuambia “uhai wetu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu”, na sio katika wingi wa vitu tulivyo navyo.
Tuombe neema ya kutumia vitu tulivyonavyo na nafasi tulionayo kwa ajili ya uzima wa milele.