Msalaba Ni Njia Ya Wokovu Na Msamaha

2025-04-13
Dominika ya Matawi
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Injili Lk 22:14-23:56 

🕊️ Tafakari ya Neno

Katika liturujia ya kanisa Dominika ya Matawi inajulikana pia kama Dominika ya mateso. Ndio mwanzo wa juma kuu, ambapo kilele chake ni adhmisho la kufa na kufufuka kwake Yesu Kristo. Maandamano katika Dominika hii yanakuwa ni ukumbusho wa kuingia kwake Kristo kwa shangwe katika mji wa Yerusalemu, (Mt 21 :6-1 1 ). Matawi yanatukumbusha kushiriki na Yesu katika mateo yake.

Somo la 1 : Somo hili linaonyesha wimbo wa mtumishi wa Bwana anayetuonyesha mafumbo ya mateso yasioelezeka yenye upendo wa Bwana ndani yake usioelezeka. Mtumishi wa Bwana anapokea mateso na magumu yote kwa Imani kubwa. Ni mwaliko kwetu sisi pia kama watumishi wa bwana, kama wana wa Mungu kupokea kwa unyenyekevu changamoto mbalimbali na mateso mbalimbali tunayopitia katika maisha yetu. Haidhuru hata kama mtu amekuudhi ama kukuenda ubaya kiasi gani, Paulo anatuambia msimlipize kisasi mwachie Mungu maana yeye asema “kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, asema Bwana. (Rum 1 2:1 9)

Somo la 2: Yesu anatudhihirishia utimilifu wa wimbo wa Mtumishi wa Bwana kwa kukubali mwenyewe kujinyenyekesha na kuitii hata kufa msalabani. Kristo anaendelea kukazia kwamba utii na unyenyekevu katika magumu yoyote ama changamoto yoyote ndio njia ya wokovu. Msalaba ndio njia pekee ya wokovu wetu. Mateso na changamoto za maisha tusizibebe wenyewe, yopo Kristo kwa ajili yetu ambaye kwa upendo wake ametupenda hadi kutoa maisha yake msalabani kwa ajili yetu. Jambo la msingi ni kumshirikisha kwa imani misalaba yetu atufanyie wepesi.

Injili: Katika Injili tunasimuliwa historia ya mateso ya Bwana kadiri yamwinjili Luka. Waenjili wote wanne wanaandika juu ya historia ya mateso ya Bwana. Upekee wa mwinjili Luka ni pale anapotufundisha kutoa msamaha katika mateso makali. Yesu anawasamehe watesi wake katikati ya maumivu makali. Anatufundisha na sisi kwamba njia pekee ya kuweza kutokulipiza kisasi kwa adui zetu ni kutoa msamaha wakati tunateseka, wakati tukiwa katika ugumu, katika mateso. Hivyo msamaha unaifanya misalaba yetu kuwa miepesi katika maisha. Katikati ya maumivu makali, Yesu anakutana na unyama, giza, ugumu wa moyo wa mwanadamu. Lakini sala yake inabadili giza hilo la roho ngumu ya mwanadamu na kuufunika kwa huruma ya Mungu. Sala yako tu ndio yenye kumbadili adui yako ama mtesi wako, mbaya wako n.k. Mapambano huongeza chuki, ugomvi, vita, kisasi, kutokusamehe, na kukosa furaha ya kipasaka. Mt. Rozi wa Lima anasema Msalaba ndio njia pekee ya Mbinguni, na Paulo anasema “Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu, tena nayatimiza katika mwiliwangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake yaani kanisa lake

 Katika Dominika ya leo ya Mateso ya Bwana, tunajifunza kwamba mateso ya Yesu ni ngazi ya wokovu wetu. Licha ya kwamba wale waliomshangilia kuingia Yerusalemu ndio waliomgeuka na kupiga kelele asulubiwe, yeye aliwasamehe. Tuombe neema ya kupokea misalaba yetu kwa imani kubwa na tuombe neema ya kuwa ngazi ya baraka, wokovu, msamaha, upendo, amani, furaha, mafanikio kwa wengine hata kama ni watesi wetu au wabaya wetu, au adui zetu. Bwana akupe amani!