Somo la Kwanza: Yer 38:4–6, 8–10
Somo la Pili: Ebr 12:1–4
Somo la Injili
Lk 12:49–53
Siku ile Yesu aliwaambia makutano: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe? Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe; mkwe na mkwe mtu.
Utangulizi
Tunapoianza safari ya imani, ni mashindano na mapambano. Hivyo lazima kusimama Imara na kufaya maamuzi magumu. Yeremia anasimamia ukweli licha ya kutakwa afe. Yesu anasema bora kumkiri yeye kuliko ndugu au wazazi. Tumwombe Mungu kupitia Mwanae, atusaidie kupigana vita vya kiroho.
HOMILIA
Somo la I: Nabii Yeremia anahukumiwa afe kwa sababu ya kuwaambia ukweli wakuu wa Yuda. Anashutumiwa kifo kwa sababu ya kuwaeleza watu waache maovu yao katika mji wa Yuda. Na hasa maovu yao katika unyanyasaji, unyonyaji na vita. Yeremia anatupwa shimoni.
Ndugu zangu wapendwa, ni wazi kuwa ukweli haupendrwi na msema kweli hapendwi. Tuko radhi auwawe. Hasa pale tunaposemwa maovu yetu. Hivyo tunajikuta tunaanguka kwenye dhambi kubwa hasa; ya kutokusema ukweli, kuuficha ukweli, kuuwa wasema ukweli, kutetea uovu, kutokusimamia imani yetu. Hivyo tunaalikwa kusimama imara tusikubali kumezwa na wimbi hilo la kushabikia uovu, kushabikia dhambi. Na Hakika tunaposimama imara na kuitetea imani yetu na ukweli, Mungu atamtuma Ebedmeleki akuokoe katika shimo la kifo.
Somo la II: Katika la pili, Waraka kwa Waebrania unatuambia, kwanza Yesu ndiye mwenye kuanzisha imani na ndiye mwenye kuitimiza ndani yetu. Tunachotakiwa kufanya ni kupigana na kushindana na dhambi, na uovu.
Jeshi la watakatifu na mashahidi ndio mfano bora wa wale waliosimamia imani yao kwa Kristo mpaka kufa. Walikubali kufa kwa ajili ya Kristo. Ndio wanaosherekea ushindi na mwanakondoo huko Mbinguni. Kwa maombezi yao wanatutia Moyo katika vita na mapambano na uovu na dhambi hapa duniani tusikate tamaa.
Injili: Katika somo la Injili Yesu anatutaka tufanya maamuzi magumu juu ya imani yetu. Haidhuru hata tukikosana na ndugu ama wazazi pale tunapokuwa na maamuzi sahihi ya Imani kwa Kristo. Wakati wa Yesu na wakati wa mafundisho yake iliwataka watu wawe na msimamo wa kuamua kumfuata Yesu ama kubaki na dini yao ya zamani. Walioamua na kumfuata walifarakana hata na familia zao, hata na wazazi wao. Huo ndio moto anaousema Yesu kuwa amekuja kuuwasha duniani. Uamuzi mgumu katika kumfuata Kristo.
Ndugu wapendwa hata na sisi uamuzi wetu katika mumfuata Kristo unaweza kutufarakanisha na ndugu, familia, wazazi n.k. Mfano mtu anapoamua kubatizwa pengine kutokea dini nyingine, kukataa matambiko ya wazee, kukataa mila potofu, kukataa kurithi mila potofu, kuamua kuwa mtawa au padre. Haya na mengine mengi yanazua mtafaruku katika familia.
Hivyo Yesu anatutaka kuchukua maamuzi magumu ya kuchagua imani sahihi ya Kumkiri Kristo na kupiga mbio kwa saburi katika mashindano na mapambano ya Imani yaliyo mbele yetu. Simama imara na Kristo atakuokoa na shimo la kifo kama alivyomwokoa nabii Yeremia.