Somo la Kwanza: Isa 66:18-21
Somo la Pili: Ebr 12:5-7, 11-13
Somo la Injili: Lk 13:22-30
Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.
Utangulizi: Katika Dominika ya leo, Mungu anatukumbusha ushiriki wa watu wote katika ufalme wa Mungu. Ufalme wa Mungu umewekwa kwa ajili yetu sote. Kuufikia ni juhudi za kila mmoja za kupita kwenye Mlango mwembamba. Na Mlango wenyewe ni Kristo Mwenyewe. Chagua Kristo, Chagua wokovu, chagua ufalme wa Mungu.
HOMILIA
Somo la I: Mungu anawaahidia utukufu wa wake watu wa Israeli, baada ya mateso mengi utumwani Babeli. Unabii huo ni wa matumaini kwamba; kwanza Mungu anatimiza ahadi yake. Pili Mungu ana malengo anapokusanya watu wake. Ni kwa ajili ya utukufu wake. Na pia baada ya kuwakusanya anawafanya mabalozi na kuwatuma kwa mataifa mengine.
Ndugu zangu, Mungu anatuokoa na kutuleta kwake ili tuitimize kazi yake ndani mwetu. Hilo linawezekana tu kwa kuwa na juhudi katika kushirikiana na Mungu katika maisha Yetu na hasa kuwaleta waliopotea kwake. Kuwaleta watu wa mataifa kwake, kuwaokoa wasiosali, kuwahubiria wasiopenda neno lake, kuwahubiria ukweli wasiopenda haki na ukweli, n.k
Somo la II: Katika somo la pili tunaambiwa, hiyo kazi ya Mungu ya kuwaambia watu watende haki na kupenda ukweli si nyepesi. Inahitaji unyenyekevu na nidhamu. Ili kwanza sisi tumrudie Mungu na ndipo tuwaongoe wengine. Kama baba anavyomwadhibu mtoto wake ili anyooke basi nasi Mungu anapotupitisha kwenye ugumu ni ili tuweze kupita kwenye mlango mwembamba.
Injili: Katika somo la Injili, Kristo anatukumbusha kwamba si kazi yetu kujua watakaookolewa. Ni vizuri kila mtu afanye juhudi mwenyewe kuingia katika mlango mwembamba kwa ajili ya wokovu wake. Kuhusu kuingia mbinguni mlango uko wazi kwa kila mtu. Tiketi yako ni juhudi yako katika sala, upendo, ukarimu, unyenyekevu, huruma, wema, haki, n.k. Kufahamu kuhusu ufalme wa mbinguni ni jambo moja, kufahamu kuhusi imani yako, imani katoliki ni jambo moja. Lakini kuwa mkatoliki na kuishi imani hiyo ndio njia ya kuuendea mlango mwembamba.
Ndugu zangu katika Dominika hii tunajifunza Mambo yafuatayo:
- Mungu anatoa nafasi na fursa kwa wote: Wokovu ni kwa wote Juhudi zako ndizo zitakazokufikisha kwenye ufalme wa Mbingu. Si kwa sababu wewe ni wa taifa fulani, nafasi fulani, kabila fulani, n.k
- Mungu anatupigania kwa shughuli maalumu ya kuwaokoa na kuwasaidia wengine. Sio kuwadhulumu, kuwanyonya, kuwaringishia, ama kuwadharau wengine. Mungu anatuinua ili tuwainue wengine (Kum 19:5).
- Mungu anatusafisha ili tuweze ku fit katika kazi yake na katika ufalme wake wa mbinguni.
- Mlango uendao kwa shetani ni mpana. Nao ndio dhuluma, rushwa, wizi, njia ya mkato, ufisadi, miungu mingine, unyanyasaji, unyamana, uonevu n.k
Wokovu wetu ni juhudi zetu katika sala, haki, amani, toba na upendo. Mungu hatatukomboa pasipo sisi kutaka. Wokovu hauji tu hivihivi. Ni lazima juhudi na jitihada ili tuweze kupita katika mlango mwembamba.