Msalaba Ndio Kipimo cha Ufuasi Wetu

2025-09-07
Dominika ya 23 Ya Mwaka, C
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Hek 9:13-19

Somo la Pili: Flm 1:9c-10, 12-17

Somo la Injili: Lk 14:25-33

Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi: Katika maisha ya mwanadamu si rahisi kumsikia mtu anafurahia mateso, tabu, shida, magumu n.k. Ni wazi mahangaiko yetu mengi kama sio yote ni kwa ajili ya kutoka katika mateso, shida, magumu n.k. Lakini Mungu amependa kupitia katika njia ya mateso ili kutupatanisha naye. Nasi bila kupitia tunayopitia na kuyapokea kwa imani, hatuwezi kumfikia Mungu.

Somo la I: Maisha yetu yote lazima kuomba kuongozwa na hekima ya kimungu. Hekima hiyo hupatikana katika sala. Tunapopata hiyo hekima ya Kimbungu ndipo tutaweza kuoanisha ya mbinguni na duniani katika yale tunayofanya kila siku. Sehemu ya kitabu cha Hekima ya Sulemani ni sehemu ya sala yake juu ya hekima ya kuweza kuoanisha maisha ya kila siku na Hekima ya Kimungu, Maisha ya mbinguni. Hekima hiyo inapatikana tu katika msalaba wa Kristo.

     Sala hasa, ya kuomba hekima ya mang’amuzi ya kiroho ndiyo inayotuwezesha kubeba magumu ya maisha yetu kama sehemu ya msalaba katika maisha yetu na kuyabeba kwa imani.

Somo la II: Msalaba ndio hekima yenyewe. Msalaba ni ishara ya msamaha. Paulo anamuombea msamaha Filemoni, na kutaka apatanishwe na bwana wake. Anamuombea arudi kwa bwana wake na ampokee sio tena kama mtumwa bali kama mwanae. Ikumbukwe mazingira anayozungumzia Paulo wakati inaandikwa hiyo barua, ilikuwa kwamba mtumwa akimtoroka bwana wake na akikamatwa anauwawa.

     Tunajifunza kwamba sheria ya kweli inaongozwa na hekima ya kimungu. Na hasa katika msamaha, tukijifunza katika msalaba ndipo tunaweza kuwa wamisionari wa Injili kama Mtume Paulo.

Injili: Katika somo la Injili, Yesu anatugeukia na kutuuliza swali, je tuko tayari kumfuata? tuko tayari kuwa wanafunzi wake?. Pengine ni rahisi kusema, Ndio, tupo tayari! Nipo tayari!. Ndio maana hata tunapokiri imani na kumkataa shetani ni rahisi lakini je? Tuko tayari kweli kumfuata Yesu?

Tuko tayari kuchukia wazazi wetu? baba na mama? – Kuna mila ambazo pengine tumerithishwa si nzuri? Je tu tayari kuacha? Kuna matambiko pengine tumerithishwa, je tupo tayari kuyaacha na kutangaza injili?. Tuko tayari kwenda kinyume na mke, watoto, ndugu, jamaa na jamii kwa ajili ya Injili?.

     Kumfuata Yesu ni kujikania mwenyewe na kuchukua msalaba na kwenda nyuma yake. Yesu ametumia lugha kali. Lakini ndivyo inavyopaswa kuwa. Ufuasi ni kujikania hata ndugu wa damu. Wokovu uliletwa kwa njia ya msalaba. Kadhalika nasi wokovu tutaupata kwa njia ya msalaba. Pengine tungependa ufuasi ambao sio wa msalaba, sio wa gharama, sio wa sadaka. Huo sio ufuasi wa kweli. Msalaba ndio kipimo cha ufuasi wetu. Ufuasi bila kujikania, bila gharama, bila msalaba ni ushabiki.

     Kila mtu ana msalaba wake. Kwa hakika sio wa mti kama wa Kalvari. Lakini inawezekana; shida za familia, magonjwa, kutokuelewana, kukosa ajira, kufeli, mitego ya shetani, uvivu, wivu, masengenyo, ulevi, ukorofi, ubinafsi n.k. Pengine ndiyo tunayopambana nayo. Pengine tumeisababisha, au tumesababishiwa na watu au mazingira. Namna ya kushinda misalaba hiyo na kuwa wamisionari waenezaji wa Injili, tumepewa katika masomo yetu ya leo:

     Kusali kuomba Hekima: kama tulivyosikia kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani.

     Kusamehe: Kuomba na kuwaombea wengine msamaha, kama Paulo anavyomwombea Onesmo kwa bwana wake.

     Kueneza habari njema katikati ya mateso: Paulo licha ya kuwa gerezani bado anakuwa balozi wa Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo.

     Kuutazama Msalaba wa Yesu: Ndio kielelezo na kipimo cha ufuasi wetu. Hakuna magumu au mateso, au dhiki, au shida au adha, au magonjwa yanayoshinda Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

     Hivyo, tuombe neema ya kuwa wafuasi kweli wa Yesu Kristo na sio washabiki tu wa imani. Tukitambua kwamba, hakuna hakuna neema bila mateso, bila msalaba hakuna njia ya mbinguni