Moyo Usio na Shukrani Hukausha Mema Yote

2025-10-12
Dominika Ya 28 Ya Mwaka, C
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: 2 Fal 5:14-17;

Somo la Pili: 2 Tim 2:8-13;

Injili: Lk 17:11-19

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi: Tunaposhukuru na kutii sauti ya Mungu, tunadhihirisha imani yetu na tunafungua mlango wa baraka na neema na rehema za Mungu. Katika Dominika ya leo tunaalikwa kufungua milango ya Baraka kwa kumshukuru Mungu katika maisha yetu.

HOTUBA

Somo la I: Katika somo la kwanza tunasimuliwa juu ya ukuu wa Mungu unaojidhihirisha katika habari za Naamani. Naamani Jemedari mpagani aliponywa ukoma wake na nabii Elisha. Baada ya kuponywa anakiri kuwa Mungu wa Israeli ana nguvu za pekee kuliko miungu yote ya Israeli. Mwenyezi Mungu daima anadhihirisha ukuu wake kwa viumbe wake.

     Kupitia mambo tunayoona ya kawaida sana, Mungu hutuongoza kufanya uzoefu wa ajabu wa nguvu zake. Hii inabaki kuwa siri ya nguvu na ufanisi wa sakramenti za kanisa, Ishara ya nje ya neema zilizofichika na wema wa Kimungu.

Somo la II: Katika somo la pili, Mtume Paulo anamkumbusha Timotheo amkumbuke Yesu Kristo aliyefufuka, uzao wa Daudi ambaye Paulo anateseka kwa ajili yake. Anamwambia “Kama tumeishi naye, tutatawala naye pia, kama tumemkataa naye atatukataa.” Utii na shukrani hutegemea imani kwa Yesu Kristo ambayo hutupa nguvu ya kuvumilia. Unapomshukuru Mungu kwa jambo la kawaida unaamini pia katika jambo lingine kubwa na kuvumilia katika mateso. Mates ohayo yanatuimarisha katika utii kwa neno la Mungu na shukrani kwa Munngu.

Injili: Mwinjili Luka anatupa simulizi la Yesu alipita katika mipaka ya Samaria na Galilaya. Kwenye sehemu ambapo wakoma walilazimishwa kuishi. Walitengwa na jamii kwa kuwa ukoma ulionekana ni ugonjwa hatari na kunajisika. Hawafungamani wala kuchangamana na wengine.

     Yesu anawaambia “nendeni Mkajionyeshe kwa Makuhani” katika kutii hilo neno wanatakasika. Kutii kwao neno la Yesu wanatakaswa. Tunapoitii sauti ya Mungu tunatakaswa. Makuhani ndio waliowathibitisha kama mwenye ukoma amepona na anaweza kurudi kwa jamii.

     Ndugu zangu wale tisa waliona ni kitu cha kawaida. Ama kwa maneno mengine walijisahau. Bali msamaria aliona ni kitu kikubwa na cha pekee katika kuponywa kwake akarudi kwa imani na moyo wa shukrani. Huruma ya Mungu iko nasi na kutuponya kila mara. Tusichukulie maisha yetu kama ni kawaida, na ni haki yetu kila tulichonacho ama kila tulichofanikiwa. Ndugu wapendwa masomo yetu yanatukumbusha mambo yafuatayo:

     Nguvu ya Mungu katika Maisha yetu: Mungu anadhihirisha uwezo wake katika kumtakasa Naamani. Msamaria pia anashuhudia uwezo wa Mungu kwa kutakaswa. Naamani na Msamaria wanatudhihirishia miujiza na uponyaji ambao ni siri kubwa ya nguvu za Mungu. Nasi Mungu anatuponya kila mara hata pasipo sisi kuona au kujua

Sauti ya Mungu Katika maisha yetu: Ni wazi kwamba Naamani aliujua mto Yordani kabla. Lakini bila sauti ya Mungu kumwongoza kupitia mtumishi wake Elisha hakujua cha kufanya. Tuisikilize sauti ya Mungu katika maisha yetu, inatuongoza katika mafanikio katika kupona. Sauti ya Mungu inasema nasi daima katika Neno lake, sakramenti zake na katika watumishi wake.

Kushukuru Daima kwa mema mengi Mungu anayotujalia: Ndugu zangu tunaweza kujihesabia haki vile tulivyo, afya, mafanikio, kufaulu, cheo, ajira, kazi, uongozi, bila kujua kuwa yupo aliyetustahilisha. Tusichukulie kawaida mafanikio katika maisha hata kama ni madogo kiasi gani, tutafanana na wale tisa, walioona ni kitu cha kawaida kupona. Tusijisahau tunapofanikiwa katika neema, baraka na rehema za Mungu:

Kutoa sadaka ni sehemu ya shukrani kwa Mungu: Naamani amedhihirisha hilo pale anaporudi kwa shukrani na kutaka kumjengea Mungu hekalu kwa kutakasika kwake. Je wewe unamshukuruje Mungu kwa mafanikio Yako?

Ndugu zangu wapenda leo tunakumbushwa kuwa na utii kwa sauti ya Mungu na amri zake na kuwa watu wa shukrani. Hiyo ndiyo namna ya kuonyesha imani yetu. Shukuru kwa kila jambo. Unaposhukuru unaomba tena. Basi daima tukumbuke kutambua uwepo wa Mungu na Kusema ‘Asante” kwa Wokovu na “Asante” kwa mema unayonijalia kupitia watu wako. Na hivyo tutajazwa mema mengi zaidi katika maisha yetu.