Usalipo Jitazame Nafsi Yako Mbele Ya Mungu

2025-10-26
Dominika ya 30 Ya Mwaka, C
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Sira 35:12-14,16-18

Somo la Pili: 2 Tim 4:6-8, 16-18

Injili: Lk 18:9-14

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Sala yenye kustahili mbele ya Mungu ni sala inayosaliwa kwa unyenyekevu na kujishusha mbele za Mungu. Leo tunakumbushwa kumwendea Mungu kwa moyo wa Toba na unyenyekevu ili sala yetu ipenye mawingu.

TAFAKARI

Somo la I: Katika somo la kwanza, Yoshua Bin Sira anatuambia sala ya mnyenyekevu hupokelewa na Mungu, huhesabiwa haki mbele ya Mungu. Sala zetu zitahesabiwa haki mbele ya Mungu pale tu tunapojishusha na kujinyenyekesha mbele za Mungu.

     Umwelezapo Mungu malalamiko yako kwa unyenyekevu na unyofu wa moyo, Mungu huyasikia. Lakini hata wewe unayemlalamikia Mungu lazima uzishike sheria zake, umtolee Mungu dhabihu ya kumshukuru, na uepuke dhuluma. Mungu daima anaangalia moyo uliopondeka na kuvunjika (Zab 51:17).

Somo la II: Sala hii ya unyenyekevu iwe ni katika nyakati zote. Paulo anaonyesha sala yake ya shukrani na unyenyekevu baada ya kutazama yale ambayo Mungu amemjalia wakati wa utume wake. Anamshukuru Mungu kwa kuilinda imani. Na sasa anamshukuru Mungu kwa kazi hiyo kwa sala. Na ana imani bado kwamba Bwana atamuokoa katika kila neno baya.

     Basi nasi kwa unyenyekevu tumlilie Mungu naye atatuokoa katika kila neno baya na kutuhifadhi hata tuufikie ufalme wake. Dhabihu pekee inayomstahilia Mungu ni kujitoa maisha yetu kwa ajili ya Kristo

Injili: Mfano wa Mfarisayo na mtoza ushuru katika sala wanaonyesha maana halisi ya sala na namna ya kusali. Ni wazi kwamba wafarisayo walikuwa ni watu waaminifu katika dini ya kiyahudi. Walikuwa wanajitenga na malimwengu. Walijitenga na wapagani. Waliongoza sala katika masinagogi, walipendwa na watu, waliongoza ibada katika majumbani. Waliwasaidia maskini hapo mwanzo, walishika sheria/torati na kutoa zaka. Mafarisayo walianza kupotoka kwa kujiona maarufu na kujiabudu. Badala ya kujitoa tena kwa maskini na wanaoteseka, waling’ang’ania sifa na heshima kwa watu. Hiki ndicho tunachokisikia katika somo la injili. Anajisahau na kujisifia mbele ya Mungu. Ndugu zangu mtoza ushuru alihesabiwa haki kwa kujishusha na kunyenyekea mbele ya Mungu kwa kujitazama nafsi yake. Tunajifunza kwamba:

     Hivyo ndugu zangu tunaalikwa kumwendea Mungu kwa Moyo wa toba na unyenyekevu, ndipo sala zetu zitahesabiwa haki mbele ya mwenyezi Mungu. Mungu atuimarisha na kutudumisha katika imani hiyo kusudi nasi mwisho tusali kwa ujasiri kama Paulo. Nimevipiga vita vilivyo vizuri imani nimeilinda.