Furahini Daima Katika Bwana

2025-12-14
Dominika ya 3 ya Majilio, Mwaka A
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap
📖 Masomo ya Dominika

Somo la kwanza: Isa 35:1-6, 10

Somo la Pili: Yak 5:7-10

Injili: Mat 11:2-11

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Ndugu zangu wapendwa leo tunaalikwa katika Dominika hii ya tatu ya Majilio Kufurahi. Bwana wetu yu karibu. Mungu anatualika tufurahi katika Bwana, katika yeye. Mwaliko huu basi utuzamishe katika kudumu katika sala na katika shukrani kwani Mungu daima anatufungulia baraka na neema zake katika maisha yetu.

 

Homilia:

Gaudete in Domino Semper” Haya ni maneno ya wimbo wa mwanzo yanayotualika tufurahi katika Bwana. Mara nyingi tunapokuwa katikati ya safari ama ya shughuli fulani tunapata matumaini na furaha. Na kurudi nyuma inakuwa ngumu. Mara nyingi tunasema, aheri tumalizie, tumeshafika nusu. Hii ndio maana pia Dominika hii imeitwa Dominika ya furaha kwamba tumekaribia Noeli, tumekaribia kumpokea Bwana.

Somo la I: Katika kufurahi huko, Nabii Isaya anatupa simulizi la Furaha mpya jangwani pale ambapo Bwana anawaonyesha njia mateka wa Babiloni wanarudi. Wanapata matumaini na furaha mpya wanapokombolewa utumwani. Bwana anawapigania, Bwana anawakomboa, Bwana anawaonnyesha mji mpya.

     Waambieni walio na hofu, jipeni Moyo, msiogope. Yesu anatuambia na sisi leo: usiogope, jipe Moyo, Utashinda Bwana yu nawe. Bwana atatenda, Bwana ametenda mema mengi kwako. Bwana atakuinua, Bwana atakuwezesha, Bwana atakupa maisha mapya. Furahi, usiogope.

Somo la II: Mungu ni mwaminifu kwa ahadi yake. Anapotuambia usiogope, usiwe na hofu, anakutaka ufanye hjambo moja tu. Uvumilie. Kwa nini anasema tuvumilie, Mungu anajua hali yako ya sasa. Katika kuvumilia huko ndipo tunapata fadhila ya imani, matumaini na udumivu katika sala. Ndio maana yakobo anatupa mfano wa mkulima mwenye kuvumilia hadi wakati wa mavuno.

     Sisi shida yetu tunataka tukipanda leo kesho tuvune, tukifungua biashara leo kesho tuwe bilionea, ndio maana michezo ya bahati nasibu, Kamari inashika kasi. Sio kweli. Maisha hayapo hivo. Na kwa kawaida njia ya mkato ni njia ya yule mwovu, ni njia ya adui, haina haki, haina usawa, haina amani, ina madhara na matokeo hasi, na yasioyompendeza Mungu na mwanadamu.

Injili: Katika somo la Injili tujiulize swali dogo. Je furaha tunaipata wapi. Yesu anawauliza wanafunzi wa Yohana swali hilo pia. Je mlienda ama mlitoka kwenda kufanya nini kwa Yohana? Kuona mazingira? kupunga upepo?, kuona watu walivyovaa, kumwona nabii?..? Yesu anawaambia wapo naye aliyezungumzwa na nabii huyo lakini bado hawajamtambua.

     Nasi tunaweza kujiuliza hilo swali. Je nimekuja kunisani kufanya nini? Kuona watu walivyopendeza, kuona mazingira, kuona kwaya wanavyoimba, kuona Mapadre, kuona kanisa linavyoendelea, kusikia wanatangaza nini, kusikiliza michango, kusalimia marafiki? Yesu anasema na kama umekuja kwa hayo! hautatoka na kitu. Kwani hutakuwa na tofauti na yule aliyekaa nyumbani akatazama misa kwa runinga.

     Kumbe leo tunakumbushwa kuja kanisani ni kukutana na Bwana na Kufurahi katika Bwana. Furahi kwa sababu umekutana na neno la Mungu, Furahi kwa sababu umekutana na Bwana Katika neno lake, katika sala, katika matoleo na zaidi sana katika Ekaristi Takatifu. Ndio maana ya Kufurahi katika Bwana tukiishia na mambo ya nje ndipo tutabaki patupu kama hao wanafunzi wa Yohane Yesu anawauliliza mmekwenda nyikani kutazama nini?

     Hivyo, tumwombe Mungu atujalie daima tufurahi katika Bwana siku zote tukimtazamia kuja kwake katika maisha yetu kwa kufungua mioyo yetu daima ili kupokea baraka zake katika kudumu katika kushika amri zake, kufurahia kusali, kukaa na Bwana, kumwomba kwa uvumilivu daima na kumshukuru kwa mema mengi anayotujalia katika maisha yetu.

                                                                          

              **************Bwana azaliwe katika mioyo yetu**************