Somo la Kwanza: Isa 7:10-14
Somo la Pili: Rom 1:1-7
Injili: Mat 1:18-24
Somo la Kwanza: Isa 7:10-14
Somo la Pili: Rom 1:1-7
Injili: Mat 1:18-24
Utangulizi
Tunapokaribia kuzaliwa kwa Yesu, anatualika tuache hofu, mashaka, mipango binafsi, na tufungue mioyo yetu kwa Mpango wa Mungu katika uwajibikaji. Kama Yosefu tunaitwa kuamini hata pale tusipoelewa kikamilifu.
Homilia
Yesu anakaribia kuzaliwa tufungue mioyo yetu atutoe wasiwasi katika kutekeleza wajibu wetu. Jina Yesu analopewa maana yake, anatuokoa katika mashaka, wasiwasi, na katika ubinafsi wetu. Ndiye anayekuja kutawala katika maisha yetu; Imanuel- Mungu pamoja nasi katika maisha yetu.
Somo la I: Katika somo la kwanza, mfalme ahazi anapokea ishara kutoka kwa Mungu. “Tazama bikira atachukua Mimba na atazaa mtoto, naye ataitwa jina lake Immanuel; Mungu pamoja nasi. Ahazi anaogopa maadui lakini Mungu anampa ishara ya matumaini makubwa kuliko hofu zake. Ahazi anatolewa hofu. Ahazi alikuwa na mashaka na hofu ya kuomba ishara. Lakini Bwana anampa ishara hiyo kubwa ya Matumaini.
Tunajifunza kuwa Mungu anatimiza ahadi yake hata pale ambapo tunashindwa kuamini, tumekata tamaa, hatuoni mbele, hatuna matumaini, n.k. Ahazi anakkataa na kutokuamini lakini Mungu anampa ishara, anampa matumaini. Pale ambapo hata na sisi tunakuwa na hofu ya kesho yetu, hatima ya familia, hatima ya kazi yangu, hatima ya taifa letu. Tunakumbushwa tu kuwa Mungu anafanya kazi hata katika mashaka yetu makubwa juu ya maisha yetu. Anakuja Immanueli mwenye kuishi ndani ya hali yetu ya maisha.
Somo la II: Mtume Paulo anatangaza Injili ya Yesu Kristo aliyeahidiwa tangu zamani na sasa amefunuliwa kwetu. Kwa maneno mengine maaguzi ya nabii Isaya yanatimia katika kuzaliwa kwa Yesu.
Katika somo Hili tunapata kila sababu ya kuamini ujio wa Bwana wetu Yesu. Na ujio huo kwetu ndio sababu ya utii kwa imani yetu na Neema ya Mungu katika maisha yetu. Neema ya Mungu katika maisha yetu inadhihirika katika kumpokea Yesu ambaye ndiye neema yenyewe katika maisha yetu. kama wakristo tunaalikwa kuishi kwa namna ambayo watu wataiona na kuonja neema ndani yetu. Yaani watu wamshuhudie Yesu katika maisha yetu na hasa pale tunapowajibika.
Injili: Katika somo la Injili tunasikia simulizi ya Yosefu mtu wa haki na muwajibikaji. Anakabiliwa na fumbo la mimba ya Maria na hatimaye kuchagua utii kwa Mungu.
Yosefu anapitia hofu, mashaka, na maamuzi yake magumu, lakini hatimaye anasikiliza na kulitii neno la Mungu.
Katika somo la injili tunajifunza kuwa:
Mungu anatekeleza mpango wake kwetu katika ukimya na unyenyekevu. Mungu anamuongoza Yosefu katika hali yake ya mahangaiko yake ya ukimya. Hii inatufundisha kuwa Mungu anafanya kazi yake katika mazingira yasioyoonekana na ambayo hata sisi hatuwezi kuyatambua hadi anapotufunulia.
Utii wa Imani Yetu unahitaji ujasiri wa kuacha mambo mipango yetu binafsi. Yosefu alitaka kuondoka na kumwacha Maria kimya kimya lakini Mungu anapangua mpango wake na kumrudisha kwa Maria. Hata wewe alipokuacha Mungu anatekeleza mpango wake kwako.
Yosefu anatufundisha pia kuwa watu wa haki. Hakutaka kuona Maria anapata shida, alitaka kutokumwaibisha, kutokukumdhuru. Hivyo anawajibika ijapokuwa hata yeye hausiki. Upendo kwa Maria unamsukuma kutokumtendea baya. Sisi pengine tunapenda kuwaabisha watu kwa kujua siri zao ama dhambi zao.
Yosefu pia anawajibika kabla na baada ya ujumbe wa Malaika. Yosefu hakurudi nyuma na zaidi baada ya kuhakikishiwa na malaika. Anamtunza Maria na Yesu hadi Mpango wa Mungu unatimilizika. Ni mfano mzuri kwa Kina baba kuwajibika katika ndoa na familia zao.
Hivyo Yosefu anatufundisha kuwa ukomavu wetu unaonekana katika kuwajibika. Tunapowajibika katika maisha yetu tunatekeleza mpango wa Mungu. Na hata tunapokosea tusisite kuwajibika na kukubali kosa. Yesu huyu anayezaliwa kwetu atujalie kutokuwa na wasiwasi katika maisha yetu na tujue kwamba katika kutimiza wajibu wetu na kuwajibika kwetu tunatekeleza mpango wa Mungu katika maisha yetu na Immanuel anaonekana katika maisha Yetu.