Ubatizo: Kuzamishwa na kushirikishwa Nguvu ya Kimungu

2026-01-11
Dominika ya Ubatizo wa Bwana
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Isai 42:1-4, 6-7

Somo la Pili: Mdo 10:34-38

Injili: Matt 3:13-17

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Ubatizo wa Bwana ni mwendelezo wa sherehe ya Epifania. Ni Mwendelezo wa ufunuo wa Mungu Mwana kwa ulimwengu. Yohane anathibitisha hilo. Mungu Roho Mtakatifu anamtambulisha kwa watu/kwetu. Na sauti ya Baba inadhihirisha hilo. Tumwombe Mungu atujalie kuishi ubatizo wetu.

Homilia

Somo la I: Katika somo la kwanza, tunasikia mtumishi wa Bwana anapokea Roho ya Bwana ili atimize kazi ya Bwana. Utimilifu wa huyu mtumishi wa Bwana tunauelewa zaidi tukiutazama ubatizo wa Yesu. Kuitimiliza haki yote. Ndicho anachoambiwa huyu mtumishi: Ametolewa kwa ajili ya Mataifa, hatalia wala kulalamika, atapata mateso lakin hata kata tamaa. Atakuwa agano na watu wa Mungu, atakuwa nuru ya mataifa, atayafunua macho ya vipofu, atawaachia wafungwa huru, na zaidi amefanya haki kwa watu. Tunaziona kazi hizo anazitimiza Yesu baada ya Ubatizo.

     Nasi tunapobatizwa tunakuwa watumishi na wana wa Mungu tunaopendezwa naye. Tunazamishwa katika Maisha ya utakatifu, katika muunganiko na Utatu mtakatifu na tunatumwa kuishi ubatizo wetu na kwa Nuru na mwanga kwa ulimwengu. Tutaushinda ulimwengu si kwa nguvu bali kwa unyenyekevu.

Somo la II: Mtume Petro katika somo la pili anatueleza kuwa Mungu hana upendeleo. Sote tu wa Mungu. Masharti ni mawili tu kwa Mungu. Kumcha Mungu na kutenda haki. Yesu baada ya Ubatizo wake anapakwa mafuta na kuanza kazi ya ukombozi ambazo tumezisikia hata katika somo la kwanza. Utume aliopewa Mtumishi wa Bwana. Kuponya na kuuokoa ulimwengu.

     Ubatizo wetu, hauishii katika ibada tu. Unatudai kuishi. Kumcha Mungu na kutenda haki. Mafuta, maji na sala na neema tunazopata katika ubatizo ni nguvu tosha ya kupambana na ibilisi na uovu na kuishi maisha ya kumcha Mungu. Tunazamishwa katika Umungu wa Kristo na kushiriki katika utume wake.

Injili: Katika somo la Injili, Yesu anazamishwa katika ubinadamu wetu kwa unyenyekevu wake. anakubali kubatizwa na Yohane na kuingia katika ubinadamu wetu. Kubatizwa kwa Yesu si kwa sababu alikuwa na dhambi ama dhambi ya asili, la hasha. Jibu analotoa Yesu- “Kutimiza haki yote” linaonyesha kuingia kwenye ushirika na mwanadamu aliyeanguka ili kusudi aweze kumkomboa. “Rightioushness” Ni neno linalotumika kuonyesha Yesu alishuka kwetu na kuingia kwenye ushirika na mwanadamu, to be in solidarity with humanity, na kutuonyesha maisha mapya katika ushirika na Utatu mtakatifu. Ndio maana kwa ubatizo anaingia kwenye maisha yetu nasi tunapobatizwa tunazamishwa kwenye ushirika na Mungu kupitia Yesu Kristo. Ndio maana tunaambiwa sasa tumekuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa.

     Hivyo Yesu Yesu anajinyenyekeza na kuungana kikamilifu na wanadamu. Ubatizo wake unafunua fumbo la Utatu Mtakatifu. Ubatizo wake unatambulisha utume wake hadharani.

     Ndugu zangu wapendwa, ubatizo wa Yesu utukumbushe ubatizo wetu. Unatukumbusha kuwa ubatizo wetu ni chanzo cha nguvu na neema ya maisha yetu ya Kikristo. Katika vurugu za duniani na uovu uliopo duniani, Mkristu anayekumbuka utambulisho wake na kuingia kwake katika muungano na Kristo hawezi kupotea ama kumezwa na malimwengu ama na shetani.

     Kwa ubatizo Mungu anatutambua sisi kama watoto wake na anatuingiza katika ushirika naye na kutupatia utume wa maisha yetu yote. Tumwombe nguvu na neema ya kuendelea kuhuisha nguvu ya sakwamenti ya ubatizo tuliyoipokea.