Furaha ya Maisha Ni kutimiza Mapenzi Ya Mungu

2026-01-18
Dominika ya Pili ya Mwaka A
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la kwanza: Isa 49:3, 5-6

Somo la Pili: 1 Kor 1:1-3

Injili: Yn 1:29-34

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Leo ni Dominika ya pili katika kipindi cha mwaka, mfululizo wa mwaka A. Dominika ya kwanza huwa ni Dominika ya Ubatizo wa Bwana. Katika masomo yetu leo, tunaalikwa kutambua kuwa “Mwanakondoo wa Mungu” ni zaidi ya Mtumishi. Ndiye aliyetimiza kwa ukamilifu mapenzi ya Baba. Tunaalikwa nasi kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yetu.

Homilia

Jumapili mara baada ya ubatizo wa Bwana, inatualika kuutambua wito wetu kama wakristu. Tumeitwa kwa ubinadamu wetu kutimiza wito wetu kama watumishi wa Bwana, kila mtu kwa nafasi yake na hali yake. Wewe na mimi tunaalikwa kuwa Yohane pale tulipo, katika nafasi zetu, kazi zetu, katika maisha yetu ya kila siku.

Somo la I: Katika somo la kwanza tunamsoma na kumsikia tena mtumishi wa Bwana. Mtumishi huyu anakuwa na sifa tafu muhimu. Moja anaaminiwa na Mungu na kuchaguliwa na Mungu. Anapokea utume na kuchaguliwa kwake na Mungu kwa kujitoa sadaka kwa wengine. Anapewa kazi/utume wa kuwa mwanga na kuuleta mwanga kwa Waisraeli.

     Mungu kwa kukuumba pia, amekuchagua, na anakuamini, anakukabidhi nawe kazi kama mtumishi wake, katika maisha yako, katika familia, kazi, jamii na kwa ulimwengu mzima. Kwa ubatizo, mwanga uliopewa ni kwa ajili ya kuwa mtumishi wa Bwana na kuwa mwanga kwa walio na wanaoeneza giza.

Somo la II:   Katika somo la pili tunasikia Paulo anathibitisha wito wake kuwa mtume. Anathibitisha unyenyekevu wake na utii wake kwa mapenzi ya Mungu. Anaelezea umuhimu wa kufanya mapenzi ya Mungu. Moja ya kutimiza mapenzi ya Mungu ni kuisha utakatifu. Utakatifu tunaupata kwa kufanya toba, kujipatanisha na Mungu. Na ni hivyo tunatangaza habari njema kwa watu kwa kuishi wito na maisha yetu kitakatifu.

Injili: Katika somo la Injili, Yohane mbatizaji anamtambulisha mwokozi kwa ulimwengu. Kwa kufanya hivo Yohane anaonyesha kuwa kazi yake imekamilika, na ametimiza kazi/mapenzi ya Mungu. Kumtayarishia njia. Ni mfano kwetu mzuri wa kupokea kazi ya Mungu, kukubali kazi ya Mungu na kumtangaza Yesu kwa ulimwengu.

     Ni wakati sasa na sisi kumtangaza Kristu kwa watu kama Yohane alivyofanya. Ni wakati nasi wa Kumwinua Yesu na kusema “Tazama Mwanakondoo wa Mungu tazama aondoaye dhambi za ulimwengu”.  Maneno hayo yanaonyesha Yesu ni zaidi ya Mtumishi wa Bwana. Anazo sifa zote za Mtumishi wa Bwana; trusted, accepted, and share to others good news. Lakini sifa Kubwa aliyo nayo “Mwanakondoo”. Hii inatupa picha ya mwanakondoo yule wa Pasaka, Kut 12. Huyo alikuwa ishara. Yesu ni Mwakondoo “wa Mungu”. Aondoaye dhambi za ulimwengu. Ana uwezo wa kuondoa dhambi. Hii ni sifa ya Mungu. Ndiye mwenye kuondoa dhambi. Hivyo huyu ni Mungu. Anabatiza kwa Roho Mtakatifu, ni Mwana wa Mungu.

     Tunaalikwa kujiuliza, Je tunampelekea dhambi zetu huyo Mwanakondoo? Au tumekuwa sugu na kukumbatia dhambi zetu. Na pengine tuna mashaka kama anao uwezo wa kutuondolea dhambi zetu na hasa kwa sakramenti ya kitubio! Yeye ni Mwanakondoo wa Mungu aondoa dhambi za ulimwengu, na anao uwezo na mamlaka na kutuondolea dhambi zetu kwa sakramenti ya kitubio (Mk 2:10).

     Ndugu wapendwa ili tuweze kutambuliwa na Mungu na kuaminika kama mtumishi wa Bwana katika somo la kwanza ni lazima tuwe wanyenyekevu kwa ubinadamu wetu mbele ya Mungu. Tunapotubu tunakuwa – trusted, (kuaminika), tunalipokea neno lake (Accepted the message), na baada ya kulipokea neno lake na kulipeleka kwa watu. Hapa ndipo tunapotambua wito ndani ya wito.

     Tumwombe Mungu atujalie tuweze kuaminika naye katika maisha yetu kwa kutimiza mapenzi yake.