Huruma ya Mungu Idhihirike Katika Maisha Yetu

2025-04-27
Dominika ya 2 ya Pasaka
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Injili Luka 24:1 -1 2

 

🕊️ Tafakari ya Neno

Siku ya Mwisho huwa ndio siku kubwa ya sikukuu (Yn 7:37-38).

Mara nyingi tunaita siku ya kilele. Katika sikukuu ya wayahudi ya vibanda, iliyochukua siku nane, siku ile ya Mwisho ilikuwa sikukuu kubwa. Hii ndio chimbuko la Dominika ya Huruma ya Mungu aliyovuviwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II. Kwamba siku zote nane tokea Dominika ya Pasaka tumekuwa tukiadhimisha sherehe ya Pasaka kwa uzito ule ule kwa siku nane, octave kwa kilatini. Hivyo siku hiyo ya mwisho tunajipatia kitu kikubwa zaida ambacho ni Huruma ya Mungu. Dominika ya Huruma Ya Mungu ilitangazwa rasmi na Papa Yohane Paulo wa II, mwaka 2 0 0 0 wakati wa kutangazwa kuwa Mtakatifu Sr. Faustina Kowalska.

Tunaimba na mzaburi 1 1 8:1 , wakati wa octava ya Pasaka kwamba “mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele”. Kwa kuwa katika midomo ya Kristo mfufuka tumepokea ujumbe mkubwa wa Huruma ya Mungu na imekabidhiwa katika huduma ya mitume kwenye chumba cha juu, walipotokewa na Yesu Mfufuka (Yn 2 0:21 -23). Amani iwe kwenu Katika somo la Injili tunathibitishiwa Huruma ya Mungu katika maneno ya Yesu. Maneno hayo yanatokea kwa msisitizo mara tatu. Maneno hayo yamebeba a) Furaha, b) Msamaha c) Faraja. Huruma ya Mungu huleta furaha tunapojua kwamba tumesamehewa bure, freely forgiven. Mitume walikuwa na woga, wasiwasi na mashaka wakajifungia ndani. Ukiachilia hofu ya Wayahudi lakini pia wamekata tamaa, waliomwomba wakae mkono wake wa kulia na kushoto, amezikwa. Yesu anapowatokea wanajawa na furaha kumwona tena Bwana. Pia wanajawa na furaha zaidi kwa maneno ya Yesu, Amani iwe kwenu. kwani wasiwasi wao ulikuwa ni kwamba atawauliza mbona mlikimbia nilipokamatwa, Petro mbona ulinikana, mbona mliniacha wakati wa mateso, lakini Yesu anawajalia msamaha kwa kuwajalia amani.

Salamu hii inawatakasa kwa msamaha wasiostahili. Hivyo Kristo mfufuka anawajalia Huruma yake na wanafarijika. Hiyo ndio furaha tunayopata kwa Yesu tunaposamehewa naye. Tunapojihisi hatupokei tena msamaha, tumefungiwa huruma yake, tumekata tamaa, tunapokosa matumaini kwa sababu ya udhaifu wetu na dhambi zetu, lakini Yesu anatuambia nenda kwa amani dhambi zako zimesamehewa. Furaha, Msamaha na faraja tunayoipata ndiyo Huruma yenyewe ya Mungu. …Wowote Mtakaowaondolea dhambi wameondolewa;… Yesu aliona furaha, msamaha na faraja hiyo isiishie tu kwa mitume bali kwa kanisa na ulimwengu mzima. Hivyo Yesu baada ya kuwapa amani, aliwavuvia Roho Mtakatifu na kuwapa mamlaka ya kuwa vyombo vya Huruma ya Mungu kwa njia ya sakramenti ya Kitubio. Mungu anawafanya mitume na waandamizi wao, maaskofu na mapadre kuwa chaneli ya Huruma yake. Pamoja na hayo, kama wabatizwa wote kwa kumpokea Roho Mtakatifu kwa matendo na maneno mema tunakuwa vyombo vya Huruma ya Mungu. Maana yake ni kwamba Mungu amelifanya kanisa kuwa chombo na alama ya upatanisho kwa Huruma ya Mungu. Hivyo tunapaswa kujiuliza, Je? tunaikimbilia hiyo huruma ya Mungu katika sakramenti ya Kitubio? na Je? tumekuwa chombo cha Huruma ya Mungu kwa wengine? Tukiwa majumbani kwetu? katika familia zetu? makazini? Katika Jumuiya zetu? na popote tunapokuwa? Au tumekuwa chanzo cha watu kukosa furaha, msamaha na faraja? Ingawa Thomaso alikuwa na mashaka Yesu hakumhukumu, bali alimruhusu ashike na aone inapobubujika Huruma ya Mungu katika ubavu wake. Damu na Maji zinazowakilishwa na miale miwili kutoka ubavu wa Yesu, unaonyesha Huruma ya Mungu kupitia sadaka ya Yesu msalabani kunakozaliwa sakwamenti za kanisa, hasa Ekaristi Takatifu adhimisho la sadaka ya Yesu Msalabani.

Thomaso anatufundisha pia wakati wa mashaka, kukata tamaa, kutokuamini, tuikimbilie Huruma ya Mungu katika sakramenti za kanisa, tuguse na tuone, nasi tuseme “Bwana wangu na Mungu wangu. Madonda yake hushinda mashaka yetu, kutokuamini kwetu, majaribu yetu, na zaidi hushinda dhambi. Yohane anatuambia katika ufunuo, Huruma ya Mungu inaonekana katika vazi la Yesu aliye mfano wa mwanadamu. Naye Yohane anaanguka na kumsujudia kwani alikuwa amekufa na sasa yu hai hata milele na milele.

Hivyo katika yeye aliyefufuka tunapokea Huruma ya Mungu. na mwito kwetu sio tu kuipokea Huruma yake bali kuishuhudia kwa wengine kwa kuwasaidia wanaoteseka, kuwa amani kwao wenye mashaka na wasio na amani, kuwa watu wa kusikiliza na zaidi kuleta faraja, furaha na msamaha kwa wengine.