Usibagaini na Shetani

2026-02-22
Dominika ya 1 ya Kwaresma
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la kwanza: Mwa 2:7-9; 3:1-7,

Somo la Pili: Rum 5:12-19

Injili: Matt 4:1-11

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi:

Tunapojikita zaidi katika matendo na sala za kwaresma, majaribu ndivyo yanavyozidi. Maisha ya Mwanadamu yanayo majaribu yanayoletwa na yule mwovu. Hapa na pale yanatuangusha. Ushindi pekee wa majaribu hayo ni katika Kristo Yesu aliyeshinda majaribu jangwani. Ee Yesu utupe nguvu ya kushinda majaribu hasa kipindi hiki cha mfungo na katika maisha yetu.

Homilia:

Somo la I: Katika somo la kwanza, kutoka kitabu cha mwanzo tunasikia anguko la mwanadamu. Mwanadamu anapoteza uhusiano wake na Mungu, anapoteza neema, anapoteza furaha aliojaliwa na Mungu, anapoteza uhusioano wake mzuri na mwanadamu mwenzake. Yote hayo yalitokana na Eva kumpa shetani nafasi na kukubali kumjaribu yeye na Adamu. Walitenda dhambi ya uasi, dhambi ya kutotii, dhambi ya kutokutii sauti ya Mungu, kutaka kuwa sawa na Mungu.

     Dhambi ya kiburi, majivuno, kutokusikiliza dhamiri zetu njema inatuondoa katika uhusiano wetu na Mungu. Inavunja ukaribu wetu na Mungu na uhusiano wetu na wenzetu. Shetani anatumia nafasi hiyo, hasa ya uhuru wetu wa kuchagua kupitia utashi wetu. Tunaposhindwa kuzitii amri za Mungu, kutii sauti za wakubwa wetu, wazazi wetu, wenzi wetu wa ndoa, viongozi wetu wa kiroho, tunatoa nafasi kwa shetani kututumia.

Somo la II: Katika somo la pili, Mtume Paulo anatupa matumaini kuwa, licha ya kwamba katika jaribu la kwanza, shetani alishinda na dhambi ikaingia ulimwenguni, lakini Mungu ana nguvu kuliko shetani. Mungu wetu ni Mungu wa Ushindi, ni Mungu wa neema, ni Mungu wa upendo.

     Mungu ameendelea kutupigania sisi wanadamu kwa upendo wake. Ametuletea neema iliyopotea kwa njia ya Yesu Kristo. Mungu ameturudishia tena uhusiano wetu na Yeye kupitia Yesu Kristo aliyechagua njia ya unyenyekevu kwa kuitiii sauti ya Baba yake. Ameshinda kiburi, majivuno, kujikweza, amemshinda shetani na vishawishi vyake. Ndio maana Kwaresma inatukumbusha kujishusha na kutambua ubinadamu wetu mbele ya Mungu kwa kuisikia sauti yake kupitia neno lake.

Injili: Katika somo la Injili, tunaona Yesu anajaribiwa na ibilisi. Ibilisi aliyemwangusha Adamu na Eva, bado anang’ang’ania kuangusha mpango wa Mungu. Anataka mpango wake ufanikiwe wa kuvuruga mpango wa ukombozi wa mwanadamu. Yesu anajaribiwa mara tatu na anashinda kwa kishindo. Shetani anamtega ili tu asitii sauti ya Baba yake bali alitii neno lake. Yesu hakumpa nafasi. Alimpa majibu ya papo kwa hapo. Hakukubali kubagaini naye.

     Mara nyingi katika Biblia, Yesu anapokutana na ibilisi, ama pepo wabaya, hatoi nafasi ya kumsililiza au kubagaini naye. Eva alifanya hivo, Ibilisi akamshinda. Yesu ameshinda kwa kutoto nafasi kwa shetani. Ndio mbinu yetu kwa ajili ya kumshinda Ibilisi, kushinda vishawishi, kushinda mitego ya adui. Usitoe nafasi ya kumsikiliza na kuzungumza na shetani.

     Katika hayo majaribu matatu yanatuonyesha pia maisha yetu na hasa safari ya kwaresma inaweza kukumbwa na majaribu na vishawishi. Katika jaribu la kwanza Yesu anajaribiwa na Ibilisi kuhusu njaa. Katika maisha yetu tunaendeshwa na chakula, kula, kuvaa na kunywa. Ibilisi anapitia humo kutushawishi. Angalia mafarakano ya chakula, kunywa, kuvaa n.k., Mambo ya kuhangaikia miili yetu.  Kufunga chakula kwaresma inatusaidia kutambua kuwa “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”

     Jaribu la pili shetani anamjaribu Yesu atumie nguvu za kimungu. Atumie uwezo wake wa kiroho kuwaagiza malaika wamdake. Kutaka Mungu afanye anavyotaka shetani. Yesu anagundua mtego wake na anamwambu usimjaribu Bwana Mungu wako. Mahitaji ya kiroho yanatudai udumivu, uvumilivu, ustahimilivu, hekima, na maongozi ya Roho wa Mungu mwenyewe. Wakati mwingine kishawishi tunachokutana nacho katika kuomba na kusali ni kwamba mbona Mungu hajibu sala yangu au ombi langu. Tunajikuta kumlazimisha Mungu afanye tunavyotaka sisi na sio kadiri ya mapenzi yake. Tukumbuke “wakati wa Mungu ndio wakati sahihi”. Sisi tumwamini na kumtegemea Mungu daima.

     Jaribu la tatu ni kuhusu mali na madaraka. Kwamba Yesu atapata mali na nguvu na madaraka akimsujudia tu shetani. Jaribu hili linatuandama kila mara katika maisha yetu kuhusu mali na madaraka. Watu wanawehuka sababu ya mali, sababu ya fedha, sababu ya madaraka. Hata inapogharimu maisha ama uhai wa mwingine, mtu yupo radhi kuliko akose mali au madara au fahari. Watu wako tayari kutoa kafara hata ndugu zao wa damu ili mradi apate mali au madaraka au cheo. Ibilisi alisahau kuwa Yesu hategemei mali za dunia, nguvu ya kisiasa, fahari ya mali. Bali anayo mamlaka juu hata ya mali. Kwaresma inatukumbusha kushinda mtego huu wa ibilisi juu ya mali, madaraka, fahari na vyeo.

     Tumwombe Mungu atujalie kutokumruhusu shetani atushawishi na kutuingiza majaribuni. Neema yake kupitia Bwana wetu Yesu Kristu ituwezeshe kumshinda shetani anapojaribu kutuangusha kwa vishawishi na mbinu zake.