Kutoka Upofu hadi Umaizi

2026-03-15
Dominika ya 4 ya Kwaresma
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: 1 Sam16:1, 6-7, 10-13

Somo la Pili: Eph 5:8-14

Injili: Yn 9:1-41

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Ndugu zangu wapendwa leo tunaadhimisha Dominika ya nne ya kwaresma. Nayo Huitwa Dominika ya Furaha. Kilatini Laetare. Hii inatupa matumaini kuwa safari yetu ya Kwaresma imefikia katikati. Tunaalikwa kufurahi kwa sababu Kristo Mwanga wetu anatufumbua macho yetu ya roho.

Homilia

Safari yetu ya toba ni safari ya kutoka upofu hadi umaizi, ufahamu, imani. Katika somo la Injili, tunaona aliyezaliwa kipofu anapata kuona kwa kukutana na Kristo, na si kuona tu anatambua kuwa ni Nabii na si Nabii tu ni Bwana. Kinyume chake, waliozaliwa wanaona wanakuwa vipofu, kwa kutokumwona Kristo Bwana kama mwanga katika maisha yao.

Somo la I: Katika somo la kwanza tunasikia Mungu anamchagua Daudi kati wa watoto wa Yese na kumpaka mafuta. Yese alitazama kwa nje kama kawaida yetu wanadamu, akawapitisha watoto wake wakubwa mbele ya samweli, lakini Bwana hakuwachagua hao. Mungu anamchagua Daudi kwa sababu ya moyo wake.

     Mungu anatazama moyo wala si sura. Jamii zetu zinawatazama watu kwa mali zao, elimu zao, hadhi zao, umri wao, vyeo, nguvu n.k. Hivyo vyote Mungu anasema havina umaizi, havina mwanga wa Kimungu ndani mwake. Mungu anaangalia moyo na anauangaza moyo kwa mwanga wake. Na hivyo thamani ya ipo kwa moyo wake na si kwa vitu.

Somo la II: Katika somo la pili, mtume Paulo anatuasa kuwa tunapobakia katika mambo ya nje, tunakuwa gizani. Na kwa ubatizo wetu tumekuwa watoto wa nuru. Tunaalikwa kutakasa mioyo yetu pale tunapokuwa katika matendo yanayozaa giza na kurudi katika matendo ya mwanga.

     Paulo anatuasa tuyakemee yanayotia giza mioyo yetu kwani yanaleta aibu. Ni kweli yale tunayofanya kwa siri tukiyaleta hadharani ni aibu na fedheha. Kwaresma ni safari ya kuchunguza maisha yetu na kuacha matendo yanayotupeleka gizani.

Injili: Katika somo la Injili tunasikia simulizi refu la Yesu kukutana na mtu aliyezaliwa kipofu. Yesu anamponya kwa kumpaka tope, na kupona kwake kunazua mjadala mrefu. Hatima yake tunaona pande mbili zilizokinzana vikali.

     Moja ni aliyezaliwa kipofu anapona, si upofu wa nje tu, bali anapata umaizi, ufahamu wa ndani, insight, na kumuona Yesu kuwa Nabii na Bwana. Yesu ndiye anayeleta Mwanga wa Kweli, ndiye mwanga halisi wa maisha yetu. Ndiye mwanga wa ulimwengu. Leo tunaalikwa kufurahi kwa sababu:

     Pili ni wanaokataa mwanga wa Kristo. Kristo amekuja ulimwenguni ili tupate kuona. Kristo ndiye Nuru ya ulimwengu. Kundi la pili la mjadala wa somo la Injili ni la Wayahudi waliokataa kusadiki kuwa Kristo ni Nabii na Bwana na ndiye aliyemponya kipofu yule. Hawa wanaukataa mwanga wa ulimwengu, wanaukataa ukweli, wanakataa kufungua mioyo yao, wanakataa umaizi, kufunguliwa ufahamu wao. Hawa wanawakilisha wale ambao:

     Yesu anasema kwamba wale wanaosema na kudai kuwa wanaona na wanajua, hubaki kuwa vipofu. Na wale wanaokiri kuwa vipofu kwa unyenyekevu hupokea mwanga wa Kristo na kumkiri kuwa Bwana na Nuru ya Maisha yao. Hivyo, tumwombe Mungu atujalie kumpokea Bwana mioyoni mwetu, tuchaguliwe kama Daudi na tuishi katika Mwanga na kuacha na yale yanayotupeleka gizani.