Somo la Kwanza Mdo 5:27b-32, 40b-41
Somo la Pili Ufu 5:11-14
Injili Yn 21:1-19
Somo la Kwanza Mdo 5:27b-32, 40b-41
Somo la Pili Ufu 5:11-14
Injili Yn 21:1-19
Yesu anatushibisha kwa neno lake na kwa Ekaristi Takatifu kisha anatutuma. Ndivyo anavyowaimarisha wanafunzi wake anapowatokea baada ya ufufuko wake.
Somo la I: Katika somo la Kwanza tunamwona Roho Mtakatifu anamjaza Petro na kumbadilisha yeye ambaye tutamsikia Yesu akimkabidhi mamlaka ya kuliongoza kanisa katika Injili. Yeye aliyekuwa akiogopa mamlaka za kiyahudi sasa anasimama mbele ya mahakama na makuu wa makuhani na kusema bila woga; “imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”. Nasi ushuhuda wetu kwa ufufuko wa Yesu ni pale tunaposimama imara katika majaribu na vitisho.
Somo la II: Somo la Pili linatuingiza katika maono ya Yesu wa Ufufuko kama mwanakondoo aliyetukuzwa mbinguni. Tunapata matumaini ya kuwa imara na kuamnini kwamba ufufuko wa Yesu ndio mlango wa maisha ya umilele, maisha ya mbinguni. Kwa ufufuko wake tunapata uhakika wa milele mbinguni. Injili: Tokeo la Yesu kwa wanafunzi wake mara ya tatu ni uthibitisho wa ufufuko wake kwa wanafunzi na kwetu. Hii inadhihirisha kwamba amefufuka kweli. Ndiye Bwana tunayemshangilia Pasaka. Yesu anadhihirisha kwamba ufufuko sio hadithi ya kutunga, sio roho kama ilivyo ya mizimu, na sio kama ufufuko wa Lazaro. Yesu Mfufuka anaishi, ni mzima, Yu hai mbinguni na duniani.
Ndio maana anawafanyia muujiza wa kupata samaki, na baada ya muujiza huo anashiriki nao mlo/kifungwa kinywa na baadae anawatuma kupitia Petro kiongozi wa mitume na kanisa. Ishara ya samaki na Kuchunga kondoo ndizo kazi za kimisoari za kanisa. Tunajifunza yafuatayo katika masomo ya leo; Kusimama Imara katika Imani: somo la kwanza linatupa msisitizo huo. Kusipatikane kitu chochote cha kututenga na Kristo. Iwe mamlaka, iwe mila zetu, iwe kazi zetu, iwe changamoto, iwe matatizo ya maisha n.k. Yesu yeye anatuita daima ‘njoni mfungue kinywa.’ Tufungue macho yetu kumwona Yesu Mfufuka: Licha ya kwamba tumesherekea ushindi wa Yesu sikukuu ya Pasaka, bado tunaweza tukawa tumesharudi kwenye mazoea yetu ya mwanzo kama wanafunzi walivyorudia kazi yao ya kawaida ya uvuvi. Yesu anatualika kufungua macho yetu na kumwona katika mafanikio yetu. Wanafunzi waliporudi tena kuvua samaki hawakufanikiwa bila Yesu. Nasi tunachokifanya bila Yesu hakitafanikiwa. Na katika jambo lolote, lazima tusema, nimeweza hili katika yeye anitiaye nguvu. Ndio kusema “Ndiye Bwana” Kutambua uwepo wa Yesu katika Maisha yetu. Yeye ndiye anayebariki mafanikio yetu, ndiye anayebariki ushindi wetu, kufaulu kwetu, kupandishwa kwetu cheo, kuajiriwa kwetu, kufaulu kwetu, kuvuna kwetu, kujenga kwetu, kupona kwetu n.k Tunakutana na Yesu Katika Karamu yake/Ekaristi Takatifu: Mwaliko uliowafanya wanafunzi wamtambue ni katika mlo, katika kifungua kinywa. Yesu mfufuka tunakutana nae katika Ekaristi Takatifu.
Hii ndio namna ambayo Yesu amejifunua kwa wanafunzi wake, hata alipokuwa njiani na wanafunzi wa Emau (Lk 24:3 0-32). Ndio mwaliko wake kwetu ‘njooni mfungue kinywa’. Ndio mwaliko wa kumtambua katika Ekaristi Takatifu. Yeye mwenyewe alisema “Mimi ndimi chakula chenye uzima…na chakula nitoacho mimi ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Ewe ndugu yangu usikubali kukosa chakula hiki. Umisionari/utume: Na baada ya kumtambua Yesu katika karamu, anatutuma kuwachunga kondoo wake.
Petro, kiongozi wa mitume, anahojiwa mara tatu kama alivyomkana Yesu mara tatu, na Yesu anamtuma. Nasi baada ya kumpokea Yesu katika Ekaristi tunaulizwa mara tatu na Yesu, Je? Wanipenda? Ishi ukristo wako kiaminifu, kuwa mwanga kwa kondoo wangu, kuwa mwanga kwa wengine. Samaki na kuchunga kondoo ndiyo ishara ya kazi ya kitume ya Kanisa tunayopewa sisi kwa ubatizo wetu kupitia Petro Vika wa Yesu aliyekabidhiwa kanisa.
Tumwombe Mungu atujalie kumtambua Yesu katika maisha yetu na hasa tunapokutana nae katika karamu yake, na kupokea utume wake kwa kuwajibika kwetu kwa Imani yetu kwa Kanisa lake. Daima Yesu hatutumi tukiwa na njaa. Anatuita kwanza, ‘njooni mfungue Kinywa’ kisha anatutuma. Bwana Awape Amani!