Kiri la Imani Ni Njia ya Huruma ya Mungu

2026-04-12
Dominika ya 2 ya Pasaka
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Mdo 2:42-47

Somo la Pili: 1 Pt 1:3-9

Injili: Yn 20:19-31

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

 Karibuni ndugu wapendwa katika dominika hii ya pili ya Pasaka. Tunapoendelea kusherekea ufufuko wa Yesu, leo tunapewa siku muhimu ya Huruma ya Mungu. Kristu anatudhihirishia kuwa upendo wake uliodhihirika katika utukufu wake unaendelea kuwa nasi kwa Njia ya Huruma Yake.

Homilia

Huruma ya Mungu inabubujika katika fumbo la Pasaka. Yesu anatuonyesha kuwa huruma yake inatoka kwenye madonda yake. Kwenye ubavu wake. Ndio maana picha yake ya Huruma ya Mungu inaonyesha ikitoka katika madonda ya Yesu. Mungu anamdhihirishia Thoma kwa kugusa Kovu la Yesu. Katika masakramenti, hasa Kitubio na Ekaristi ndipo Huruma yake inakuja kwetu.

Somo la I: Katika somo la kwanza tunaona wanafunzi wanatiwa nguvu katika ushirika, katika umoja, katika kuumega mkate. Walishiriki pamoja maisha ya ukristo na kilichowaleta pamoja ni Ekatisti Takatifu, kuumega mkate. Huruma ya Mungu ilijidhihirisha kwao kwa njia ya Ekaristi Takatifu na katika kusali pamoja. Kiri la imani yao lilionekana katika kupendana, ushirika, kusaidiana.

Somo la II: Katika somo la pili ufufuko wa Yesu unatupa tumaini la uzima wa milele. Urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka. Hivyo madhumuni ya mateso wanayopitia wakristo kwa sasa si kitu wakilinganisha na Heri ya maisha ya mbinguni.

     Hata sisi tunapaswa kuushuhudia ufufuko wa Kristo hata kama ni katika mateso , ili mwisho tupate nasi kuurithi ufalme wa Mungu.

Injili: Somo la Injili limegawanyika sehemu tatu. Sehemu ya Kwanza inamuhusu Yesu Mfufuka kuwatokea mitume na kuweka sakramenti ya Kitubio, ondoleo la dhambi. Kanisa ndipo linapopata nguvu kwa njia ya sakramenti tunazamishwa katika huruma ya Mungu. Tunazamishwa katika ukristo. Mtu hupokea uzima mpya katika Kristo.

     Sehemu ya Pili inatuonyesha Yesu anawatokea mitume kwa mara ya pili na katika hilo kunatokea kiri la Toma. Kiri la Toma linaweka wazi kuwa Kristo ni mtu kweli na Mungu kweli. Na hili linatuondolea Mashaka dhidi ya ufufuko wa Yesu na linatuondolea mashaka pia dhidi ya huruma ya Mungu kwetu kupitia mateso, kifo na ufufuko wa Yesu.

     Sehemu ya tatu tunaonyeshwa umuhimu wa mapokeo ya Kanisa. Mwandishi anatuonyesha kuwa kanisa limepewa nafasi ya kuweka utaratibu wake kupitia mafunuo ya Kristu mfufuka. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya mafundisho ya kanisa ambayo hayajaandikwa katika Biblia na yapo katika vyanzo vingine.

     Hivyo ndugu zangu huruma ya Mungu inajidhihirisha katika sehemu muhimu katika kanisa. Katika sakramenti ya Kitubio, Katika kushiriki Misa takatifu na kupokea Ekaristi Takatifu, Katika kusali kwa nia za Baba Mtakatifu, katika kusamehe waliotupa majeraha, katika kufanya matendo ya huruma. Tumwombe mtakatifu Faustina aliyetokewa na Yesu na kueneza ibada ya huruma ya Mungu atujalie tuweze kuipokea Huruma ya Mungu katika maisha Yetu.