Mungu Katika Uumbaji, Msalaba na Dhamiri Zetu

2026-05-31
Dominika ya Utatu Mtakatifu
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la kwanza: Kut 34:4-6, 8-9

Somo la Pili: 2 Kor 13:11-13

Injili: Yn 3:16-18

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Leo tunasherekea fumbo la Utatu Mtakatifu. Mungu ndiye anayejifunua kwetu katika uumbaji, katika Msalaba, ndani ya Kanisa na katika dhamiri zetu. Na katika yote hayo, Mungu ni Mmoja katika nafsi tatu. Tumwombe atujalie kuona uwepo wake katika maisha yetu, katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Homilia

Utatu Mtakatifu unajifunua kwetu katika historia ya wokovu katika Upendo. Upendo unaotujali na kutuweka huru kutoka katika utumwa. Leo tunasherekea fumbo la imani yetu. Mungu alivyo. Mungu mmoja katika nafsi tatu. Katika maisha yetu ya imani, jambo la kwanza wazazi ama walimu wetu wametufundisha ni ishara ya msalaba. Inamtambulisha Mungu kwetu kuwa ametuumba, ametukomboa na anatutakasa.

Somo la I: Katika somo la Kwanza Mungu anajifunua kwa Musa ndani ya wingu. Mungu anashuka ndani ya wingu. Wingu katika Biblia linatambulisha Ukuu wa Mungu, Utukufu wa Mungu, Ulinzi na maongozi ya Mungu, Utakatifu wa Mungu. Musa anasujudia kufunuliwa huko kwa Mungu katika wingu. Anatambua huruma yake, fadhili zake, wingi wa rehema zake na kweli yake. Na anatambulisha watu wa Israeli kuwa wenye shingo ngumu. Anaonyesha ubinadamu wetu mbele ya Mungu. Lakini bado Mungu anaungama kwa Mungu atutwae kuwa urithi wake. Anamuonyesha Mungu kuwa ndiye Muumba wetu, sisi tu mali yake.

Somo la II: Katika somo la pili, tunaona kuwa Paulo anadhihirisha Huruma ya Mungu inavyotufikia kwa njia ya Yesu Kristo kupitia Roho Mtakatifu. Huruma na pendo la Mungu ambalo Musa aliwaombea wana wa Israeli kwa Mungu inadhihirika katika Utatu Mtakatifu. Kupitia Utatu Mtakatifu, Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na Pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu vinadhihirisha kwamba ukombozi wetu ni kazi ya Utatu Mtakatifu. Matunda yake ni furaha, amani na upendo.

Injili: Kati Wainjili wote wanne, Mwinjili Yohane ndiye anayezungumzia zaidi fumbo la muunganiko wa Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Maneno ambayo amekuwa akitumia ni “aliyeniona mimi amemwona baba” “mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu” (Yn 16). Leo anadhihirisha kuwa Mungu amemtuma mwana Ulimwenguni ili ulimwengu, sisi tuokolewe katika Yeye. Mwinjili Yohane anafunua wazi kazi ya mwana pekee wa Mungu katika kuukomboa ulimwengu. Hivyo ni Mungu mwana Katika Msalaba. Katika Ukombozi, katika Sakramenti, katika kanisa. Hivyo Mungu anajifunua kwetu kupitia Msalaba uliotukomboa sisi kupitia mwanae pekee aliyetundikwa Msalabani.

     Katika Fumbo la Utatu Mtakatifu tunajifunza kwamba: Mungu ni mmoja katika nafsi tatu. Na anajifunua kwetu kama apendavyo yeye katika hizo nafsi tatu. Katika uumbaji, katika ukombozi na katika kutakasa dhamiri zetu. Kila ilipo nafsi moja nyingine zipo pia. Hata kama moja haionekani ama ipo kimya.

     Tunaposema ni fumbo ni kwamba linahitaji Imani. Kwa ubinadamu wetu tunabaki bado tunamumunya maneno. Lakini kwa macho ya Imani tunaweza kuling’amua na kulielewa.

     Kwa fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu anakuwa karibu zaidi na sisi, katika maisha yetu, katika kazi zetu, katika masomo yetu, biashara zetu, katika utawa wetu katika ukristo wetu : ndio maana tunautukuza utatu katika kila tunaposali: Ishara ya msalaba, sala ya atukuzwe, sala ya zetu tunazipeleka kwa Mungu kupitia Roho Mtakatifu. Na zaidi ya yote tunaadhimisha Ekaristi takatifu katika utatu mtakatifu.

     Hili fumbo litakuwa gumu kwetu endapo tunajitenga na Upendo wa Mungu – ambao yeye mwenyewe anajifunua kwetu. Tunapokuwa katika hali ya dhambi, katika chuki, katika mafarakano, kutokuelewana, kutokusikilizana, kutokusaidiana, kutokujaliana, kutokusaidiana n.k mambo hayo yanapingana na umoja tunaouadhimisha katika Utatu Mtakatifu.

     Hivyo ndugu zangu tunapoishi katika upendo, katika kushika amri tunatambua fumbo hili katika maisha yetu. Hatutasali tena sala zetu kwa mazoea tutazisali kwa kuusifu na kuutukuza ukuu wa Mungu katika utatu Mtakatifu.